Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam Sheikh Humam Hammudi, Rais wa Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq, ameielezea fatwa ya Jihadi Kifai iliyotolewa na Marjaiyya ya Kidini kuwa ni “ilhamu ya Kiungu”, na akaashiria kwamba; Hashdu al-Shaabi ni mwakilishi wa “mradi wa Marjaiyya”.
Sheikh Humam Hammudi alisema katika “Kikao cha Mazungumzo”: “Fatwa ya Jihadi Kifai ilikuwa ilhamu ya Kiungu kwa Marjaiyya jasiri, ambayo ndani yake ilijengwa dira iliyo wazi kwa ajili ya mustakabali. Fatwa hiyo ilizalisha usalama kutoka katikati ya janga, urahisi kutoka katika ugumu, na ikajenga mshikamano na ushindi kutoka katika mgawanyiko.”
Aliongeza kuwa: “Daesh ni mradi wa Kizayuni, katika uhalifu ambao kundi hili lilifanya huko Speicher na maeneo mengine, ilidhihirika sura nyeusi ya matwaghuti kama Hitler, Netanyahu, Saddam na chama cha Baath, pamoja na fikra ya mauaji, ubaguzi wa kitaifa na ugaidi.”
Sheikh Hammudi pia alimshukuru Ayatullah al-Udhma Sistani kwa kuiokoa nchi kupitia fatwa yake, na akawashukuru wananchi waliotikia wito wa fatwa hiyo kwa dhamiri yao ya Kiiraqi, vilevile aliwashukuru wote waliotoa mchango katika kumaliza mradi mchafu zaidi uliokuwa ukilenga uwepo wa taifa la Iraq, kuusambaratisha Umma wa Kiislamu na kuichafua sura ya Uislamu.
Rais wa Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq alisisitiza kwamba; Hashdu al-Shaabi, kupitia kujitolea kwake, ushujaa wake na uimara wa imani yake, iliweza katika kipindi cha miaka mitatu kuandika ushindi na mafanikio ambayo leo yanafundishwa hata nje ya nchi, baada ya dunia kudhani kwamba vita hivyo vingechukua miaka mingi zaidi.
Aliongeza kuwa: “Ni lazima Hashdu al-Shaabi iendelee kuwa mradi wa Marjaiyya ili Iraq ibaki huru, yenye kujitegemea na yenye watu wenye heshima, na ili ibaki mbali na utawala wa vyama vya kisiasa na matumizi ya kisiasa.”
Sheikh Hammudi alieleza matumaini yake kwamba Taasisi ya Hashdu al-Shaabi iwe kama alivyoitaka Ayatullah al-Udhma Sistani, kama ambavyo wananchi wameiweka imani yao ndani yake, na kama inavyotarajiwa kuwa; na pia iwe na kiwango cha juu kabisa cha mafunzo, hisia ya uwajibikaji na ushirikiano na vikosi vingine vya usalama.
Aidha alisema: “Kufichuliwa kwa kiini kimoja cha chama cha Baath ambacho kilikuwa kinapanga kumlenga mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa pamoja na maafisa waandamizi, kunathibitisha kwamba; mradi wa Baath bado haujamalizika, kwa hiyo, wananchi wetu wanapaswa kuwa macho, kwa sababu adui yao bado anawavizia.”
Maoni yako